Baada ya ligi kurejea, Juni 14 Simba itaanza na Ruvu Shooting katika mchezo ambao utapigwa uwanja wa Taifa
Kiungo mshambuliaji Miraji Athumani ambaye amerejea kikosini baada ya kupona majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu, huenda akawa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachoshuka dimbani siku hiyo
Hii ni habari mbaya kusikia kwa Ruvu Shooting kwani ni huyu huyu Miraji ambaye aliwaangamiza katika mchezo wa duru ya kwanza ambao ulipigwa uwanja wa Uhuru
Katika mchezo huo ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, Miraji aliweka kambani mabao mawili huku bao la tatu likifungwa na beki Tairone Da Silva
Miraji alipata majeraha kwenye mchezo huo ambayo yalimuweka nje kwa zaidi ya miezi mitano, atakuwa na nafasi ya kuanza nao tena
Kocha Mkuu wa Simba Sven vandenbroeck amesema Miraji ameonyesha kiwango kizuri mazoezini, anaamini ataiongezea makali safu yake ya ushambuliaji ambayo inaongoza na kinara Meddie Kagere aliyefunga mabao 19 na John Bocco aliyefunga mabao matatu msimu huu
Bocco naye alikaa nje kwa muda mrefu kabla ya kurejea kikosini mwezi Januari