Afisa Habari wa klabu ya Simba Haji Manara amesema kauli ya Rais wa nchi Dk John Magufuli imewapa faraja zaidi kuwa sasa wana uhakika watatetea ubingwa wao kwa msimu wa tatu mfululizo
Jana Rais Magufuli akiwa mjini Chato, alisema kuwa pengine wiki hii anaweza kuruhusu shughuli za michezo nchini ziendelee pamoja na kufungua vyuo baada ya kujiridhisha na kupungua kwa kasi ya maambukizi ya virusi vya corona
Rais Magufuli alisema wagonjwa wa corona wameendelea kupungua katika vituo mbalimbali ambavyo wanahifadhiwa
"Kama hali itaendelea hivi hadi wiki ijayo nimepanga kufungua vyuo ili wanafunzi wetu waendelee kusoma. Pia nimepanga kuruhusu michezo kwa sababu michezo ni sehemu ya burudani, Maisha lazima yaendelee," alisema
Manara amesema kauli hiyo ya Mkuu wa nchi imewapa uhakika kuwa wakae tayari kumalizia ngwe iliyobaki ili kusherehekea ubingwa wa tatu mfululizo
"Tunamshukuru sana Mh Rais Magufuli kwani kauli yake imetuhakikishia kuwa wakati wowote ligi itarejea na tutakuwa na uhakika wa kutetea ubingwa wetu kwa msimu wa tatu mfululizo. Tulikuwa na wasiwasi kama msimu ungefutwa Wanasimba tungeumia sana kwani wakati ligi inasimama tulikuwa tukiongoza kwa alama nyingi dhidi ya washindani wetu," amesema Manara
"Tutahitaji kushinda mechi tano kati ya kumi zilizobaki ili tuweze kutetea ubingwa wetu, ni jambo ambalo tutalifanikisha pasipo na shaka"