Uongozi wa klabu ya Simba umesema hakuna ofa yoyote waliyopokea kwa ajili ya wachezaji wao mshambuliaji Meddie Kagere na kiungo Jonas Mkude ambao wamehusishwa na timu za Levante na TP Mazembe
Hivi karibuni Wakala wa Kagere Patrick Gakumba alidai kupokea mwaliko kutoka klabu ya Levante inayoshiriki ligi kuu ya Hispania, La Liga ikimtaka Kagere
Aidha juzi vyombo mbalimbali vya habari hapa Tanzania na nje ya nchi viliripoti kuwa vilabu vya TP Mazembe, Al Ahly na Mamelodi Sundowns vimeonyesha nia ya kutaka kumsajili Mkude

Afisa Habari wa klabu ya Simba Haji Manara amesema klabu ya Simba inafanya kazi kwa utaratibu, suala la wachezaji hao kuwaniwa na vigogo hao wa soka halijafika mezani kwao
"Mpaka sasa hatujapokea ofa yoyote kuhusu wachezaji hao. Sisi tunafanya kazi kwa utaratibu unaoeleweka, kama ofa zingekuwa mezani mimi kama Msemaji wa klabu ningekuwa mtu wa kwanza kutaarifiwa ili kuwajuza Wanasimba"
"Hivyo mpaka wakati huu naongea, nakuhakikishia hakuna ofa iliyofika mezani kwetu," amesema Manara
Kagere na Mkude wote bado wana mkataba wa mwaka mmoja na mabingwa hao wa nchi