Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck tayari amewasilisha mapendekezo ya usajili kwa ajili ya kikosi chake cha msimu ujao
Sven ambaye alijiunga na Simba mwezi Novemba 2019, amesema usajili wa wachezaji aliowapendekeza utaifanya timu yake iwe imara zaidi
"Tuna timu nzuri ambayo haihitaji marekebisho makubwa. Usajili tutakaofanya utazingatia zaidi kuimarisha sehemu zenye mapungufu"
"Tunataka kwenye kila nafasi tuwe na angalau wachezaji wawili ambao wana uwezo unaolingana ili hata ikitokea mmoja anakosekana, hatuathiriki," amesema Mbelgiji huyo ambaye yuko nchini kipindi chote cha ligi kusimama kutokana na corona
Hivi karibuni Mtendaji Mkuu wa Simba Senzo Mazingisa alieleza kupokea mapendekezo ya Sven ambapo amesema wameanza kuifanyia kazi ripoti yake
"Hatuna wasiwasi kuwapata wachezaji wote wa ndani kwani tuna fungu la kutosha. Labda kidogo kwa wachezaji wa nje ambao mahitaji yao yanakuwa tofauti kidogo. Lakini lengo letu ni kuhakikisha tunawapa wachezaji wote waliotakiwa na Mwalimu," alisema Senzo
Baadhi ya nyota wanaohusishwa kuwaniwa na Simba ni pamoja na Reliants Lusajo, Lucas Kikoti, Baraka Majogoro, Bakari Mwamnyeto, Iddy Mobby na Sixtus Sabilo kwa wachezaji wanocheza ndani
Nyota wa nje wanaotajwatajwa Simba ni pamoja na Justin Shonga nyota wa Orlando Pirates, Joash Onyango, beki wa kati wa timu ya Taifa ya Kenya na mshambuliaji kinara wa mabao ligi kuu ya DR Congo Mpiana Mozizi wa FC Lupopo