Wiki iliyopita, Wizara ya Habari Utamaduni,Sanaa na Michezo, ililiagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha kunakuwa na ukomo wenye tija wa wanasoka wa kigeni, ili kupata wachezaji wenye viwango bora wanaocheza ligi mbalimbali hapa nchini
Akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo bungeni, Waziri wa wizara hiyo, Dk.Harrison Mwakyembe alisema licha ya uwepo wa lundo ya wachezaji wengi wa kigeni hapa nchini kwa sasa, wenye ubora ni wachache
Agizo hilo la Serikali liliibua sintofahamu miongoni mwa wadau wa soka nchini ambao wengi wamehofia kama idadi ya nyota wa kigeni itapunguzwa, inaweza kuwa na athari kwa maendeleo ya soka nchini
Leo Mkurugenzi wa Michezo Yusufu Singo, ametoa ufafanuzi kuwa Serikali haijaweka ukomo kama ilivyotafsiriwa na wengi
Amesema Serikali imeibua mjadala huo kwa wadau ili watoe maoni yao
"Serikali haijatoa ukomo wa wachezaji kutoka nje kushiriki michezo hapa nchini bali imeibua mjadala kwa wadau ili watoe maoni yao," amesema