Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesisitiza kuwa vilabu vitakavyosajili wachezaji wa kigeni ni lazima wahakikishe wachezaji hao wana ubora na wanacheza timu za Mataifa wanayotoka
TFF imesema kuwa hawatatoa vibali kwa wachezaji ambao hawatakidhi kigezo hicho
Mkurugenzi wa ufundi wa TFF, Oscar Milambo amesema katika tathmini yao waliyofanya, wamebaini kuna idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni wamesajiliwa nchini lakini uwezo wao ni wa kawaida
"Baadhi ya timu zimetumia fedha nyingi kusajili wachezaji wa kigeni ambao uwezo wao hauwafikii hata baadhi ya nyota wa ndani. Sasa ili kuboresha Ligi yetu, tutaweka kipengele katika kanuni zetu na kukifanyia kazi wakati wa usajili," alisema Milambo
Hivi karibuni Waziri mwenye dhamana ya Michezo Dk Harrison Mwakyembe aliliagiza Baraza la Michezo na Taifa (BMT) kutunga sheria itakayoweka ukomo wa wachezaji wa kigeni huku kukiwa na uwezekano mkubwa kuwa idadi ya nyota 10 wa kigeni itapunguzwa