Nahodha wa timu ya Coastal Union, Bakari Mwamnyeto amesema yupo tayari kujiunga na klabu yoyote ndani na nje ya Tanzania ikiwemo klabu ya Simba ingawa kwa sasa anaheshimu mkataba wake.
Mwamnyeto amekuwa akihusishwa kuwaniwa na vilabu vya Simba na Yanga ambapo inaelezwa tayari Simba imemalizana na Coastal Union kuhusu nyota huyo
Hata hivyo uongozi wa Coastal Union hivi karibuni ulikanusha taarifa hizo
Mwamnyeto amesema kwa sasa akili yake ipo katika kuisaidia timu yake ya Coastal Union na anaheshimu mkataba aliokuwa nao
Beki huyo wa timu ya Taifa amesema yupo tayari kujiunga na timu yoyote itakayoonyesha nia ya kuhitaji huduma yake
“Hakuna timu yoyote ambayo imenifuata kufanya mazungumzo na wala hakuna waliokubaliana na klabu yangu," amesema Mwamnyeto
Beki huyo mwenye umri wa miaka 22 amesema malengo yake ni kucheza soka nje ya nchi ili siku moja atimize ndoto zake alizojiwekea lakini klabu itakayofikia vigezo na masharti yake basi atafanya nayo kazi.