Kiungo fundi Clatous Chama 'Mwamba wa Lusaka' siku za karibuni ametawala vyombo vya habari baada ya kumuingiza matatani Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela aliyedai timu yake kuwa katika mazungumzo ya kumsajili bila ya kuushirikisha uongozi wa Simba unaommiliki mchezaji huyo
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Chama alikanusha kilichosemwa na Mwakalebela na kusisitiza kuwa yeye ni mchezaji halali wa Simba, akiwa na mwaka mmoja kwenye mkataba wake ingawa uongozi wa Simba unafanya jitihada kumpa mkataba mwingine utakaombakisha Msimbazi kwa muda mrefu zaidi
Jana Chama ambaye yuko kwao Zambia, alifunguka zaidi ambapo alibainisha kuwa katika historia yake ya kusakata kabumbu, hatalisahau bao alilowafunga ndugu zake Nkana Fc kwenye michuano ya ligi ya mabingwa mwaka juzi
Bao hilo alilofunga kwenye dakika ya 90, liliipeleka Simba hatua ya makundi michuano ya ligi ya mabingwa ambako pia ilifanikiwa kutinga robo fainali
Simba iliichapa Nkana mabao 3-1 hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3
Ni Chama pia aliyeipeleka Simba hatua ya robo fainali kwa bao lake mchezo dhidi ya AS Vita kuipa Simba ushindi wa mabao 2-1
Chama amesema anaendelea kufanya mazoezi binafsi ili kujiweka sawa kuendeleza makali yake pale ligi itakaporejea