Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema hatima ya kuendelea kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu wa mwaka 2019/20 bado haijajulikana kutokana tamko jipya lililotolewa na serikali la kusimamisha michezo kwa muda usiojulikana
Mapema wiki hii, serikali ilitoa tamko la kutoruhusu mikusanyiko ikiwamo Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na mashindano mengine mbalimbali ili kuendelea kujikinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona (COVID 19).
Awali TFF ilisema endapo hali ya maambukizi itakuwa haijaimarika, Ligi Kuu Bara inaweza kurejea, lakini itachezwa bila ya mashabiki, uamuzi ambao ulionekana kupingwa na baadhi ya timu.
Mmoja wa viongozi wa TFF amefichua kuwa wako katika mazungumzo na viongozi wa serikali kuhusiana na tathmini iliyopo ya ugonjwa huo ambao umesimamisha pia ligi mbalimbali duniani.
Kiongozi huyo amesema kuwa bado hakuna uamuzi mpya uliochukuliwa mpaka jana na hii inalenga kuweka mbele maslahi ya afya za wadau wake.
"Bado tunayafanyia kazi kwa kuangalia hali iliyopo, tunashukuru tunafanya kazi kwa karibu na serikali, mamlaka za nchi," alisema kwa kifupi kiongozi huyo.
Alisema bado hakuna maoni au mapendekezo yoyote yaliyowasilishwa na klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kuhusiana na nini kifanyike ili kumaliza msimu huu.
"Hapana, hakuna klabu yoyote iliyowasilisha maoni," Afisa huyo wa TFF alinukuliwa na gazeti la Nipashe
Mkuu wa idara ya habari na Mawasiliano klabu ya Simba Haji Manara, anaamini klabu hiyo ina nafasi ya kuchukua ubingwa katika mazingira yoyote ambayo yatajitokeza
Simba iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imejikusanyia alama 71, alama 17 zaidi ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili
Mechi 10 zimesalia kukamilisha msimu, ambapo ligi ikirejea Simba itahitaji kushinda mechi tano tu kutwaa ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo