Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba Alhaji Ismail Aden Rage, amesisitiza kwamba klabu hiyo kongwe hapa nchini imeweka historia nyingi ambazo wapinzani wao Yanga hawawezi na hawata thubutu kuzivunja.
Rage amebainisha kuwa moja kati ya historia iliyowekwa na Simba ni kuweka kambi ya siku 45 nchini Brazil kujiandaa na ligi mwanzoni mwa miaka ya 80 huku Yanga wakijitutumua lakini walikaa kambi ya siku 8 tu nchini humo.
Lakini pia Simba pia ndiyo klabu pekee iliyokuwa na ubavu wa kumsajili mchezaji yeyote waliokuwa wanamuhitaji kutokana na msuli mkubwa wa kifedha waliokuwa nao kiasi cha kuzifanya klabu nyingine kuwa wanyonge linapokuja suala la usajili wakati huo.
Pia amesema Simba ndiyo klabu iliyokuwa ikizifunga magoli mengi klabu nyingine ilizokuwa ikikutana nazo kwenye mashindano mbalimbali.
Historia nyingine ambayo Simba iliweka ni umafya wa kupora wachezaji kutoka kwa wapinzani wao Yanga, ingawa mara chache walikumbana na wakati mgumu kutoka kwa makomandoo watiifu wa klabu pinzani, ikiwemo kushindwa kumsajili mchezaji Makumbi Juma 'homa ya jiji' waliyejaribu kumpora kutoka mikononi mwa Yanga