Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck amemvulia kofia mshambuliaji wa timu hiyo Meddie Kagere kuwa ni wa kipekee
Kagere ndiye kinara wa mabao ligi kuu ya Vodacom akiwa ametupia kambani mabao 19
Mwamba huyo kutoka Rwanda yuko katika nafasi nzuri ya kutwaa kiatu cha dhahabu kwa msimu wa pili mfululizo
Sven amesema kuwa huwa anashangazwa na uwezo wa kagere, ni mchezaji anayejituma, amemtumia katika mechi nyingi kulinganisha na wachezaji wengine
Sven raia wa Ubelgiji, amesema kuwa alianza kumtumia Kagere kwenye mechi yake ya kwanza mbele ya Lipuli ambapo walishinda kwa mabao 4-0, huku mshambuliaji huyo akitupia bao moja.
"Ni mshambuliaji ambaye nimemtumia kwenye mechi nyingi kwa kuwa nilimkuta akiwa fiti na mechi yake ya kwanza alifunga, hili ni jambo ambalo linamaanisha kwamba ni mtu wa kazi kweli ndani ya uwanja, hataki masihara," amesema Sven
Kwa sasa Kagere yuko nchini Rwanda ambako alirejea kutimiza majukumu ya timu ya Taifa
Hata hivyo ameshindwa kusafiri kutokana na nchi hiyo kufunga mipaka katika kudhibiti kasi ya maambukizi ya virusi vya corona
Uamuzi kama huo umechukuliwa na Serikali ya Tanzania ambayo imesitisha safari zote za ndege kutoka nje ya nchi
Hivyo ni wazi Kagere pamoja na nyota wengine wa Simba ambao wako nje ya nchi watalazimika kusubiri mpaka pale janga la corona litakapotulia