Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba Ismail Aden Rage amesema kama kiongozi wa ngazi ya juu kwenye timu ya mpira, unapaswa kuwa makini na chochote unachozungumza mbele ya waandishi wa habari
Amesema alichokifanya Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela kudai kufanya mazungumzo na kiungo mwenye mkataba Simba Clatous Chama, ingawa baadae alijitokeza hadharani na kuomba radhi akidai ni utani, ni makosa makubwa sana
Hata hivyo Rage amesema kutokana na utamaduni uliojengwa baina ya vilabu vya Simba na Yanga, anaamini jambo hilo litamalizwa kiungwana
"Kiongozi au mtu yeyote anapaswa kufikiria cha kuzungumza kabla hajafanya hivyo, Mwakalebela ni kiongozi mkubwa katika mpira kwa sababu alishafanya kazi ndani ya TFF, inawezekana ikawa ni kweli alikuwa anaongea kimasikhara japo kwa nafasi aliyo nayo, hakupaswa kufanya vile.
"Kwa sababu amekiri mbele za watu kuwa amekosa, asamehewe tu ili maisha mengine yaendelee. Leo wamefanya Yanga, kesho inaweza kutokea watu wengine kama Mwakalebela ndani ya Simba wakafanya kosa lingine, " amesema Rage
Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Mzee Hassan Dalali ambaye pia aliwahi kuhudumu kama Mwenyekiti wa Simba
"Chochote kitakacho zungumzwa na Mwenyekiti, Katibu au Makamu Mwenyekiti wa timu katika vyombo vya habari, kitachukuliwa kwa umakini na kisheria, kuna adhabu itamkuta, lakini kwa kuwa amekiri, tena mbele za watu na kuomba msamaha, viongozi wa Simba wamsamehe tu, bila shaka hatakuja kurudia tena"
Tayari kesi ya Mwakalebela imewasilishwa kwa Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji ya TFF baada ya uongozi wa Simba kuwasilisha malalamiko TFF