Mlinda lano namba moja wa Simba Aishi Manula amesema kuwa mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Okwi ataendelea kukumbukwa kutokana na mambo makubwa aliyoifanyia klabu ya Simba na anaamini bado ana nafasi ya kurudi tena kuendeleza pale alipoishia.
Manula amesema kila mchezaji ndani ya Simba ana ubora wake, lakini Okwi ni mchezaji wa kipekee kuwahi kuichezea Simba, kwani alifanya mambo makubwa na kucheza kwa kiwango cha juu kwa muda wote aliovaa jezi ya wekundu wa Msimbazi
Okwi alijiunga na Simba kwa mara ya kwanza 2010 akitokea Sc Villa, kisha akatimka mwaka 2013 kwenda Etoile du Sahel, kisha SC Villa, Young Africans, kisha 2014 akarudi tena Simba
Akaondoka 2017 kwenda SonderjyskE ya Denmark, akaenda Sc Villa na kurudi tena Simba 2017 na 2019, akatua Al Ittihad Alexandria Club ya Misri
"Pengo la Emmanuel Okwi haliwezi kuzibika kirahisi kwenye kikosi chetu na bado tunahitaji huduma yake. Lakini siyo kwamba waliopo sasa hawana ubora bali kila mchezaji ana ubora wake na ubora wa Okwi ni tofauti na ubora wa mchezaji mwingine yeyote, hivyo hakutatokea mbadala," Manula alinukuliwa na GPL
Bila shaka mashabiki wa Simba watampokea kwa furaha mwamba huyo kutoka nchini Uganda kama ungozi utaamua kumrejesha Msimbazi kwa mara ya tatu