Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela ameiomba radhi klabu ya Simba huku akikanusha kuwa klabu yake haijafanya mazungumzo na kiungo fundi Clatous Chama 'Mwamba wa Lusaka'
Kiongozi huyo wa Yanga amedai kuwa alikuwa akifanya utani na hakumaanisha alichoeleza Yanga kuanza mazungumzo ya kutaka kumsajili Chama
"Nichukue nafasi hii kuwaomba msamaha Simba Sports Club na wanachama wa Yanga SC kuhusu kauli yangu juu ya kutaka kumsajili Claotous Chama"
"Nilikuwa nafanya utani kama wao walivyokuwa wanafanya kwa Tshishimbi ila kiukweli mchezaji huyo sijazungumza nae. Nilizidisha utani na naahidi jambo hili halitojitokeza tena," amesema
Mwakalebela ameomba radhi saa chache baada ya uongozi wa klabu ya Simba kutangaza kupeleka malalamiko TFF kwa kitendo cha klabu ya Yanga kutangaza kutaka kumsajili Chama ambaye mkataba wake na Simba ni zaidi ya miezi sita
Mapema leo, Msemaji wa Simba, Haji Manara alikanusha taarifa kuhusu mkataba wa kiungo wao Clatous Chama kumalizika mwaka huu, akisisitiza kuwa mkataba wa Mzambia huyo utamalizika mwezi Juni mwaka 2021.
Manara kupitia Wasafi FM alitoa onyo wa timu yoyote inayomuhitaji mchezaji huyo kufuata taratibu na kuacha kufanya naye mazungumzo yoyote kuhusu usajili wakati huu kwakuwa ni kinyume na kanuni za FIFA.
Pamoja na hilo, Manara hakuacha kurusha dongo kwa watani wao wa jadi ambao wamekuwa wakitajwa kumuwania mchezaji huyo, akisema kuwa hawana uwezo wa kumlipa mshahara hivyo ni jambo lisilowezekana kwa Chama kuondoka Simba kwenda Yanga.
"Amefunga goli lililotupeleka hatua ya makundi, amefunga goli lililoingia robo fainali, unajua tumeingiza kiasi gani kwa kuingia robo fainali ya klabu bingwa? Kwahiyo sisi tunajua na kuthamini zaidi umuhimu wa Chama kuliko hao", alisema Manara