Kiungo mshambuliaji wa Simba Miraji Athumani amemaliza program ya mazoezi binafsi hivyo yuko tayari kuanza mazoezi ya timu
Nyota huyo aliyetua Simba kutoka klabu ya Lipuli Fc mwanzoni mwa msimu, amekosekana dimbani kwa zaidi ya miezi minne kutokana na jeraha la kifundo cha mguu
Miraji amesema kwa sasa yuko tayari kuanza mazoezi magumu akisubiri ruhusa kutoka kwa madaktari wake baada ya kumfanyia vipimo
"Nimemaliza program ya mazoezi niliyokuwa nimepewa. Kwa sasa najisikia vizuri kabisa sisikii maumivu yoyote. Nafurahi kurejea uwanjani baada ya kukosekana kwa muda mrefu. Nawaahidi mashabiki watafurahi kwani sitawaangusha," alisema Miraji
Miraji alicheza mechi 10 tu za mwanzoni mwa msimu akifanikiwa kufunga mabao sita na kutoa pasi mbili za mabao
Sven afurahia kurejea kwake
Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck amesema kurejea kwa mshambuliaji huyo ni habari njema kwani ataimarisha safu yake ya ushambuliaji
Amesema Miraji atakuwa msaada mkubwa kwa safu yake ya ushambuliaji inayowategemea nyota wawili Meddie Kagere na John Bocco
"Miraji ni mtu niliyekuwa namuangalia sana kuweza kutuongezea nguvu kwenye safu yetu ya ushambuliaji. Ninamtegemea zaidi kuja kuwasaidia Bocco na Kagere ambao ndio washambuliaji pekee waliokuwepo," amesema
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Sven kufanya kazi na Miraji kwani Mbelgiji huyo alianza majukumu yake kunako klabu ya Simba wakati Miraji akiwa tayari ameshaumia