Uongozi wa klabu ya Coastal Union umekanusha taarifa za kuwa wamemalizana na uongozi wa Simba kuhusu usajili wa beki kisiki ambaye ni nahodha wa timu hiyo Bakari Mwamnyeto
Mwenyekiti wa Coastal Union Steven Mnguto amesema Mwamnyeto bado ana mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo na bado hawajapokea ofa kutoka kwa timu yoyote
"Taarifa za kuwa tumemalizana na Simba kuhusu Mwamnyeto hazina ukweli wowote,hatujapokea ofa rasmi kutoka kwao," amesema
Naye wakala wa mchezaji huyo Kassa Mussa aliyewahi kutamba kunako Coastal Union na timu ya taifa, amesisitiza kuwa timu inayomtaka mteja wake inapaswa kwenda kumalizana na Coastal Union
"Bakari hajafanya makubaliano na timu yoyote, kinachoendelea kwenye vyombo vya habari ni uvumi tu, kuna timu iliwahi kunitafuta na kutaka kutoa fedha za awali lakini nilipinga suala hilo, na mimi siwezi kufanya kitu chochote bila kuhakikisha kwanza timu inayomtaka Bakari inamalizana kwanza na Coastal Union ambao ndiyo wamiliki halali wa mchezaji huyo kwa sasa," alisema Kassa
Inaelezwa uongozi wa Simba uliwasilisha maombi kwa Coastal Union wakitaka kumsajili beki huyo kinda mwenye umri wa miaka 22
Tetesi zilizopo ni kuwa Coastal Union wanataka dau la usajili linalofikia Milioni 100 ili kumuachia nyota huyo