Winga wa Simba Shiza Kichuya inadaiwa amechoshwa na kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza Simba
Kichuya alisajiliwa na Simba kipindi cha disha dogo la Januari mwaka huu, akiwa kama mchezaji huru, akitokea Pharco ya Misri.
Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa pamoja na kurejeshwa Msimbazi, Kichuya amekuwa akiendekeza ‘ufalme’ wake aliokuwa nao enzi hizo kabla ya kutimkia Misri
Kutokana na hali hiyo, amejikuta akishindwa kupandisha kiwango chake na mwisho wa siku, kusotea benchi, huku wenzake wakizidi kupeta, wakiiwezesha timu hiyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa za ndani zinadai kitendo cha Kichuya kutopangwa, kimeonekana kumkera mno winga huyo na kuja juu, akishinikiza apangwe
"Kichuya kiwango chake kimeshuka kwa kuwa kule alikokuwa alikuwa hachezi, matokeo yake hapangwi halafu analalamika eti kwanini Luis Miquissone anapangwa, yeye hapangwi.
"Ameambiwa ajitume mazoezini arudishe kiwango chake ndio apangwe na si vinginevyo"
Kabla ya kutimkia Misri, Kichuya alijijengea jina Msimbazi kutokana na cheche zake uwanjani, zaidi akijipatia maujiko kwa kuifunga Yanga kila walipokutana nayo.