Kocha Msaidizi wa Simba Selemani Matola amewasisitiza wachezaji wake kutobweteka na badala yake wafanye mazoezi nyumbani ya kutengeneza mwili ili kulinda kasi waliyokuwa nayo awali.
Akizungumza Dar es Salaam, Matola alisema wachezaji watakaporudi kujiandaa na michezo ijayo, watajaribiwa na ikiwa itabainika kuwa kuna ambaye hakufanya mazoezi, basi itabidi kuandaliwa programu maalumu.
"Tulipokutana, tuliwasisitizia umuhimu wa mazoezi ya kujenga mwili wanapokuwa nyumbani ili wakirudi wasiwe wageni tena,”alisema Matola aliyejiunga na wekundu hao kwenye dirisha dogo la usajili akitokea Polisi Tanzania.
Alisema amekuwa akiwafuatilia na kuzungumza nao kuwasisitiza mazoezi hayo kwa sababu, kwa sasa ni vigumu kukusanyika kutokana na hatari ya kuenea kwa virusi vya corona.
Sio Simba tu ambao wamekuwa wakihimiza wachezaji kufanya mazoezi, bali klabu mbalimbali zimekuwa zikifanya hivyo, kwa ajili ya kuwakumbusha wachezaji kulinda viwango vyao.
Kipindi hiki ligi imesimama kufuatia maelekezo ya serikali kwa ajili ya kuepusha mikusanyiko ya watu inayoweza kusababisha kuenea zaidi kwa corona.
Tangu ligi kusimama zaidi ya wiki mbili zilizopita, wekundu wa Msimbazi Simba wamekuwa wakiongoza ligi kwa pointi 71 ikiziacha timu nyingine mbali kwa tofauti ya pointi 17 dhidi ya Azam iliyopo katika nafasi ya pili na Yanga ya tatu.