Miongoni mwa matukio yanayowauma mashabiki wa Simba mpaka leo ni kushindwa kutwaa Kombe la CAF katika uwanja wake wa nyumbani baada ya kufungwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Simba ilishindwa kutwaa taji hilo katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru), Jumamosi, Novemba 26, 1993.
Simba kabla ya kucheza na Stella Abidjan, ilianza michuano hiyo kwa kuitoa Ferroviario de Maputo ya Msumbiji kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka suluhu mjini Mwanza katika raundi ya kwanza.
Katika raundi ya pili, Simba iliitoa Manzini Wanderers ya Swaziland kwa jumla ya mabao 2-0. Katika mchezo wa robo fainali ikainyuka klabu ya Al Harrach ya Algeria kwa mabao 3-2 na katika mchezo wa nusu fainali iliiondosha Atletico Sports Aviacao ya Angola kwa jumla ya mabao 3-1.
Simba baada ya kushinda katika mchezo wa nusu fainali ndio hapo sasa ilipocheza na Stella Abidjan na kushuhudia Kombe la CAF likiondoka katika ardhi ya Tanzania na kupanda ndege kuelekea Ivory Coast.
Mashabiki wa Simba ambao walikuwa wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi, walikuwa na kila dalili ya matumaini ya kutwaa taji hilo kabla ya mechi kuchezwa.
Katika kile kilichoonekana kuwa na uhakika wa kutwaa kombe hilo, zilitengenezwa kanga ambazo zilikuwa zinaashiria kuwa Simba ndiyo bingwa, lakini ndoto hiyo ilizimwa na Desre Kouome katika dakika ya 17 ya mchezo alipofunga bao la kwanza.
Katika dakika ya 77 ya kipindi cha pili wakati Jean Ball ‘Boli Zozo’ alipofunga bao la pili na hivyo Simba kutoka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam vichwa chini baada ya kufungwa mabao hayo mawili kwa sifuri.
Mabao hayo yalifuta ndoto ya Simba ya kutwaa kwa mara ya kwanza kombe hilo na pia mabao hayo yaliwakosesha wachezaji wa Simba kupata magari aina ya KIA, ambayo waliahidiwa na mfadhili wao mkuu, Azim Dewji.
Simba ambayo ilikuwa na kikosi ambacho kilikuwa kikiundwa na wachezaji nyota, kilitoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa awali uliofanyika Jumamosi Novemba 14, 1993
Kikosi cha Simba kiliwakilishwa na kipa Mohamed Mwameja, Kasongo Athumani, Rashid Abdallah, Godwin Aswile, George Masatu, Iddi Seleiman, George Lucas, Hussein Marsha, Malota Soma/Michael Paul, Edward Chumila (marehemu)/Thomas Kipese na Damian Mrisho ‘Kimti’ (marehemu)