Kiungo wa Kimataifa wa Kenya anayewatumikia mabingwa wa nchi, Simba Francis Kahata amesema kwa tathmini yake aliyofanya, Ligi ya Tanzania ni Bora kuliko Ligi ya Kenya
Kahata aliyejiunga na Simba mwanzoni mwa msimu akitokea klabu ya Gor Mahia, amesema uwepo wa wadhamini kwenye Ligi pamoja na vilabu unaifanya Ligi ya Tanzania kuizidi ile ya Kenya ambayo mara kwa mara imegubikwa na malalamiko ya wachezaji kukosa mishahara kwa muda mrefu
"Kwa mtizamo wangu Ligi ya Tanzania ni bora kuliko ligi ya Kenya. Ligi ya Tanzania ina wadhamini wengi ukilinganisha na Kenya ambako hakuna wadhamini," amefunguka Kahata
"Kwa Kenya ni kawaida wachezaji kukosa mishahara mpaka miezi mitatu kutoka kwenye timu zao wakati tangu nimejiunga na Simba sijawahi kuona changamoto hiyo"
Klabu ya Gor Mahia ambayo Kahata alitokea, inakabiliwa na changamoto za kiuchumi ambapo inaelezwa kwa zaidi ya miezi minne wachezaji wake hawajalipwa mishahara
Mwezi uliopita baada ya Serikali ya Kenya kusimamisha ligi kutokana na changamoto ya virusi vya Corona, wachezaji wa timu hiyo kila mmoja alipewa fedha ya kujikimu ambayo ni sawa na Tsh 66,000/- fedha ya Kitanzania!