Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, amewataka Wanasimba kuwa wavumilivu na wenye nguvu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao, Asha Muhaji
Wadau wa soka nchini jana walijitokeza kwa wingi katika maziko ya aliyekuwa mwandishi mkongwe wa habari ambaye alizikwa katika makaburi ya Mwinyimkuu yaliyopo Magomeni, jijini Dar es Salaam
Akizungumza kwenye maziko ya Mwanahabari huyo Manara alisema Tasnia ya habari, klabu ya Simba na Tanzania kwa ujumla imepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwa soka la Tanzania
Manara amesema njia sahihi ya kumuenzi ni kuendeleza yale yote mema aliyokuwa akiyafanya enzi za uhai wake
"Kwa niaba ya uongozi wa klabu ya Simba inayoongozwa na Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa, tunawapa pole familia ya Asha Muhaji, tunatambua mchango wake katika tasnia ya habari hasa upande wa michezo.
"Asha pia ndiye mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki na Kati kuwa ofisa habari wa klabu kubwa," alisema Manara akimzungumzia marehemu ambaye ezi za uhai wake aliwahi kuwa msemaji wa klabu ya Simba.
"Tunapaswa kuyaenzi yale yote mazuri aliyokuwa akiyafanya, hiyo ndio njia sahihi ya kuendelea kumkumbuka mpendwa wetu.."
Asha ambaye alizaliwa mwaka 1974, alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa siku chache kwa ajili ya matibabu kabla ya mauti kumfika.
Enzi za uhai wake, Asha aliwahi kulitumikia Shirika la Posta nchini, kisha magazeti ya Majira na Spoti Starehe mwanzoni mwa miaka ya 1990 kabla ya kuhamia Uhuru na Mzalendo na baadaye Bingwa, Dimba, Mtanzania na Rai, huku kwa upande wa Msemaji wa Klabu ya Simba, akiifanya kazi hiyo kipindi cha uongozi wa Alhaj Ismail Aden Rage, mwaka 2014.
Lakini pia Asha atakumbukwa kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha hivi karibuni baada ya kuwa miongoni mwa kundi la waandishi wa habari la kuhamasisha ushindi kwa timu ya Taifa, Taifa Stars.