Huku timu yake ikiwa katika nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema kikosi chake kimejiandaa kuweka historia kwenye ligi hiyo kwa kumaliza na idadi kubwa ya pointi msimu huu
Simba ambao pia ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo imesimama kwa muda kutokana na kujiepusha kwa maambukizi wa virusi vya ugonjwa wa corona, imecheza mechi 28 na imejikusanyia pointi 71 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 na Yanga pointi 51, lakini ikiwa na mchezo mmoja pungufu.
Wekundu wa Msimbazi wamebakisha mechi 10 na endapo watashinda zote watafikisha pointi 101, lakini ili kujihakikisha ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo, kikosi hicho kinahitaji pointi 14 na kufikisha pointi 85, ambazo hazitafikiwa na klabu nyingine yoyote kwenye ligi hiyo msimu huu.
Hata hivyo, Sven ameweka wazi kupoteza mechi dhidi ya Yanga ni sehemu ya matokeo ya mchezo wa soka, na kuwataka mashabiki wa klabu hiyo kutoendelea kuumia.
Mbelgiji huyo amesema wanahitaji kupata ushindi katika mechi hizo 10 zilizosalia ili kutimiza malengo yao.
Sven alisema anafahamu mechi zote zilizobaki zitakuwa na ushindani mkubwa kwa sababu kila upande utaingia uwanjani ukiwa na malengo yake na hali hiyo huongeza ugumu.
"Nina furaha kuona tuko katika nafasi nzuri, lakini bado hatujamaliza kazi, mechi zilizobaki ni nyingi na tunatakiwa kushinda, muhimu ni kuendelea kujipanga ili kuweka rekodi na historia, tunaweza kufanya hivyo kama tutakuwa imara zaidi," alisema Sven.
Naye Kocha Msaidizi, Selemani Matola, alisema kikosi chao hakitapunguza kasi na mara ligi itakaporejea, watahitaji kushinda kila mchezo ulioko mbele yao.
"Tunataka kutetea ubingwa kwa heshima, pia tunataka kumaliza msimu kwa kishindo, hatutabweteka, tunajua msimu huu timu zitakazoteremka daraja zimeongezeka, hivyo ushindani utakuwa hadi siku ya mwisho," alisema Matola.
Kiungo na nahodha huyo wa zamani wa Simba, alisema kikosi chao kilifanya mazoezi jana asubuhi kama kawaida, lakini mchana walitarajia kukutana na uongozi wa klabu hiyo ili kujadili hatima ya kusimamisha programu kutokana na taharuki ya virusi vya corona (COVID-19) ambavyo vimeshaingia nchini.