Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba Mohammed Dewji 'Mo' ameeleza kufurahishwa na ari na upambanaji wanaoonyesha wachezaji wa Simba katika mechi za hivi karibuni
Mo amempongeza kocha mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck na benchi lake la ufundi kuwa wanafanya kazi nzuri
Mo ametaka ari hiyo ikaendelezwe kwenye mchezo wa keshokutwa dhidi ya Yanga ili kuhakikisha wanatimiza azma yao ya kutwaa ubingwa mapema
"Hongera kocha Sven kwa kazi nzuri. Kwa kweli wachezaji wetu wanajituma kwenye michezo yote tunayocheza. Sasa tujipange kwa mchezo wa jumapili na watani wetu. Lengo letu ni kuwa Mabingwa! Isha’Allah tutafanikiwa," ameandika Mo kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii
Sven aahidi burudani kwa mashabiki
Nae Sven amesema siku ya Jumapili itakuwa ya kipekee kwa wachezaji wake kwani watakuwa na nafasi ya kuwapa furaha maelfu ya mashabiki wao watakaofurika uwanja wa Taifa pamoja na wale watakaowashuhudia kupitia runinga zao
Sven amesema amewapa ujumbe wachezaji wake kuwa wafurahie, wajitume na wawape furaha mashabiki wao kwa kuibuka na ushindi
Baada ya kuwakosakosa kwenye mchezo wa kwanza na kulazimishwa sare ya mabao 2-2, Jumapili itakuwa nafasi nyingine kwa Simba kumaliza kazi mapema