Katika Kuhakikisha wanafikia malengo, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck amesema wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi dhidi ya Azam FC itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa
Simba wanaongoza Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na alama 65 baada ya mechi 25, wamepania kuhakikisha mchezo dhidi ya Azam unakuwa ni maandalizi kwa ajili ya kukabiliana na mahasimu wao Yanga hapo Jumapili wiki hii.
Mkufunzi wa Simba Sven Vandenbroeck amesema anatambua mchezo utakuwa mgumu, lakini anaamini matokeo ya ushindi katika michezo mitano iliyopita ni ishara nzuri katika mchezo huo kupata alama tatu.
Amesema yuko makini kukisuka kikosi chake kuhakikisha kila wanapomaliza mchezo wanakuwa na maandalizi ya mchezo unaofuata.
"Kila kitu ni hatua na kwa sasa tulipo si sehemu mbaya, tunahitaji kuona tunapata matokeo mazuri yatakayotufanya tuzidi kuwa imara," alisema kocha huyo.
Mbelgiji huyo alisema malengo yao ni kufanya vizuri katika michezo iliyopo mbele yao ikiwamo huu wa Azam ambao ni mazoezi tosha kuelekea mechi dhidi ya Yanga.
Aidha, amebainisha kuwa kwa sasa hawadharau timu yoyote wanayokutana nayo kutokana na kuhitaji kufanya vizuri na kupata pointi kila mechi kwa michezo iliyobaki