Nahodha wa Simba John Bocco amesema matokeo mazuri waliyopata kwenye mchezo dhidi ya Biashara United jana, yalitokana na ushirikiano mzuri wa kitimu walionao wachezaji
Akizungumza baada ya mchezo huo uliomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, Bocco amesema ushindi unazidi kuweka vizuri lengo lao la kutwaa ubingwa
"Tunamshukuru Mwenye ez Mungu tumeweza kupata ushindi. Tumecheza vizuri kipindi cha kwanza na kuwa bora zaidi kipindi cha pili, ushirikiano baina yetu wachezaji umekuwa sababu ya sisi kuondoka na pointi tatu"
"Tumeshaachana na mchezo huu tunajipanga kwa mchezo wa FA dhidi Stand mkoani Shinyanga. Lengo letu ni kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye michuano hiyo pia," alisema Bocco
Amsifu Miquissone
Bocco amemsifu nyota mpya wa timu hiyo Luis Miquissone kuwa ni mchezaji mzuri ambaye ataipa Simba mafanikio siku za usoni
"Ni mchezaji mzuri, anaonyesha uwezo mkubwa uwanjani, umri wake bado ni mdogo nadhani ataisaidia Simba msimu huu na misimu ijayo," alisema Bocco
Miquissone alifunga moja ya mabao ya Simba huku akitengeneza bao moja lililowekwa kambani na Meddie Kagere