Uongozi wa klabu ya Simba umewataka mashabiki wake kuwa na utulivu na kuendelea kuiunga mkono timu yao kuhakikisha wanatetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo
Afisa Habari wa Simba Haji Manara amesema mashabiki wanapaswa kuiunga mkono timu katika hali zote, na sio kuipenda wakati inashinda na kuitelekeza inapofungwa
"Pamoja na ukweli kuwa sisi (Simba) ndio timu bora hapa Tanzania na pengine tuna kila sababu ya kushinda kila mchezo, lakini soka haliko hivyo, kuna wakati matokeo huwa tofauti. Inapotokea tumefungwa tusianzishe migogoro isiyo na msingi, tuiunge mkono timu yetu ili kuhakikisha tunashinda mchezo unaofuata," amesema Manara
Baada ya Simba kufungwa na JKT Tanzania juzi, presha ya mashabiki kwa uongozi wa Simba imekuwa kubwa wakitaka mabadiliko ya benchi la ufundi
Mashabiki wengi wanadai kuwa timu haichezi vizuri tangu alipotimuliwa kocha Patrick Aussems na kuletwa Sven Vandenbroeck
Licha ya kushinda michezo mitano mfululizo kabla ya kupoteza juzi, kiwango cha mabingwa hao wa nchi kilionekana kuwa chini huku baadhi ya michezo wakilazimika kusubiri mpaka dakika za majeruhi kushinda