Wakati wakiendelea kukosa huduma za mawinga wake wapya Luis Miquisone na Shiza Kichuya, Simba wanashuka katika Uwanja wa Taifa leo ikiwa na lengo la kuvuna pointi tatu dhidi ya 'Maafande' wa Jeshi la Polisi Tanzania ili kufikisha pointi 50 kuelekea 100 walizolenga kuzifikia msimu huu
Hadi sasa Simba ina pointi 47 ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara, na mechi hiyo ya leo ni ya kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo yenye timu 20.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara amebainisha kuwa lengo lao msimu huu ni kuweka rekodi mpya kwa kuwa timu ya kwanza kufikisha pointi 100.
"Simba ni timu ya rekodi, tunataka ubingwa na ponti 100, kesho (leo) tunataka kufikia nusu ya lengo, hakuna timu iliyowahi kufikisha pointi 100," Manara alisema.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, Simba watashuka uwanjani katika mechi hiyo wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union, wakati Polisi Tanzania iliwafunga JKT Tanzania bao 1-0, kwenye mchezo ambao ulimalizika siku ya pili kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.
Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema mechi hiyo itakuwa ngumu licha ya kwamba wachezaji wengi walioko katika kikosi cha Polisi Tanzania anawafahamu na wamepitia katika 'mikono yake
Matola alisema mara nyingi makocha wanapata changamoto wanapokutana na timu zao za zamani na kwa kuzingatia hilo, amewaandaa Simba kupambana kwa dakika zote za mechi hiyo ya kiporo.
"Ligi ni ngumu na hakuna mechi ndogo, tumejiandaa kupambana kama tulivyopambana katika michezo iliyopita, lengo letu ni kuendelea kushinda na kujiimarisha pale juu katika msimamo, walioko chini yetu wanapambana kutufikia, sisi tunatakiwa tuongeze mbio," Matola alisema.
Naye Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania, Malale Hamsini, amesema anajua Simba ni moja ya timu ngumu, lakini vijana wake wamejiandaa kuwakabili na hawana wasiwasi wowote kuelekea mchezo huo.
Malale alisema ushindi walioupata dhidi ya JKT Tanzania umewasaidia kuongeza nguvu na wanaamini wanaweza 'kuwasimamisha' Simba katika mchezo huo.
"Sisi tumekuja kusaka pointi, tutapambana na kucheza kwa utulivu, unapokuwa ugenini halafu unacheza na Simba ni lazima uingie na mbinu mpya, usicheze kama unavyocheza kila siku, tutaingia tofauti, malengo yetu ni kupata ushindi," alisema Hamsini.
Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munisi, alisema kikosi chake kimekuja kuendeleza operesheni 'chukua pointi' kama kilivyofanya kilipokutana na Yanga mapema mwanzo wa msimu.
"Tunaijua Simba, tunajua nguvu zao ziko wapi na tunajua upungufu wao yalipo, tumewasoma, kikubwa tuwaombee uzima vijana wetu waje kutekeleza kile tulichodhamiria," Munisi alisema.
Alimtaja golikipa wao mpya Peter Manyika ameshapata ITC na anaweza kucheza katika mchezo huo wa leo endapo benchi la ufundi litaamua kumtumia.