Pamoja na kuendelea kupata mafanikio katika uwekezaji wake ulioweka kwenye klabu ya Simba, Bilionea Mohammed Dewji 'Mo' amesema ana ndoto ya kuwekeza kwenye soka katika Afrika Mashariki hasa kwa kuanzia nchi za Uganda na Kenya
Hata hivyo amefafanua kwa sasa bado anahitaji kukamilisha malengo aliyojiwekea katika uwekezaji wa klabu ya Simba
Mo amefafanua mambo kadhaa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter ambao aliendesha mjadala na kujibu maswali mbalimbali ya wadau wa soka ukanda wa Afrika Mashariki
Akijibu ombi la Faiswar Kamoga kutoka Uganda ambaye alimuomba Mfanyabiashara huyo kuwekeza soka nchini humo, Dewji alisema kuwa yuko tayari ingawa sio Uganda pekee yake bali Afrika nzima na lazima hilo lipate baraka za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
"Ninapendezwa mno kuwekeza katika mpira wa miguu barani kote kwa kuanzia Uganda na Kenya. Hata hivyo natakiwa kufanya kwanza kazi ya nyumbani kabla sijashughulika na lolote na ninafahamu kanuni katika nchi hizo na masharti ya FIFA juu ya masuala ya mgongano wa kimaslahi," alijibu Dewji.
Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mosese47 aliyetaka kufahamu iwapo anapata hasara au uwekezaji huo hauna faida yoyote kwake, Dewji ameendelea kusisitiza kuwa uwekezaji katika soka alioufanya ndani ya Simba haumpi faida yoyote.
"Duniani kwenye mpira hakuna faida! Sana sana Afrika. Hivyo lilivyokuja suala la kuwekeza Simba, sikuangalia kutengeneza pesa. Nilikuja kuleta mabadiliko kwenye mfumo, ili iendeshwe kitaalamu na baadae kuleta ushindani kwa hali ya juu"
Mo anamiliki hisa asilimia 49 za kampuni ya Simba, yeye akiwa msimamizi Mkuu wa Shughuli zote za maendeleo ya klabu hiyo