Kocha Mkuu wa Simba Sven Vandenbroeck anahitaji kufanya kazi kuirejesha Simba kwenye ubora wake kwani dalili ambazo timu inaonyesha sasa sio nzuri
Tunaamini Simba ndio timu yenye wachezaji bora hapa Tanzania, kwa misimu miwili mfululizo mashabiki wa Simba wamekuwa wakifurahia soka safi kutoka kwa mabingwa hao wa nchi
Lakini kwa sasa ni wazi Simba haichezi vile ambavyo mashabiki wamezoea kuiona. Imekuwa na mchezo wa vipindi, leo inacheza vizuri kesho vibaya, kiufupi hakuna mwendelezo
Timu inacheza taratibu sana lakini pia kumekuwa na makosa mengi sana kwenye safu ya ulinzi
Yawezekana mabadiliko ya mfumo yamechangia, wakati mwingine wachezaji wakiwa wamezoea mfumo A inawachukua muda kuweza kuzoea mfumo mwingine
Kwa michezo mitano mfululizo Simba imeruhusu angalau bao moja kwenye kila mchezo, sio takwimu za kufurahisha
Timu inapigania kutetea ubingwa wake kwa msimu wa tatu mfululizo ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao
Ni wakati huu ambao timu inapaswa kuimarika ili kuwa na uhakika wa kufanya vizuri kwenye michuano hiyo kwani kutokana na mabadiliko ya kalenda ya CAF, ligi ya mabingwa itaanza kabla ya msimu mpya wa ligi kuu
Baada ya ligi kumalizika mwishoni mwa mwezi May, hakutakuwa na muda wa kutosha kuandaa timu, hivyo maandalizi ni hayahaya ya kwenye ligi
Lakini kwa tathmini rahisi tu mpaka sasa mabadiliko ya benchi la ufundi ni kama yameirudisha Simba nyuma badala ya kuipeleka mbele