Bao la usiku lililowekwa kambani na Meddie Kagere limeihakikishia Simba kuondoka na alama zote tatu kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom dhidi ya Namungo Fc
Ulikuwa ni mchezo ambao Simba ilihitaji kutumia uzoefu wake kupata ushindi dhidi ya Namungo iliyotoa upinzani mkali
Simba ndio iliyoanza kupata bao la kuongoza kupitia kwa Francis Kahata kabla Bigirimana Blaise hajaisawazishia Namungo
Lakini haikuchukua muda mrefu kwa Simba kupata bao la pili kwa shuti kali la Hassani Dilunga
Changamoto ya safu ya ulinzi pengine inahitaji kuangaliwa kwa jicho tofauti na kocha Sven Vandenbroeck kwani imeendelea kufanya makosa na kuruhusu washambuliaji wa timu pinzani kutumia nafasi chache wanazotengeneza
Bao alilofunga Lucas Kikoti kuwasawazishia Namungo Fc kwa mara ya pili lilitokana na uzembe, wachezaji kuchelewa kuziba nafasi hivyo kumpa Kikoti muda wa kujiandaa kupiga shuti akiwa nje ya 18
Ni mchezo ambao Simba ilitawala kwa muda mwingi lakini Namungo walitumia vyema makosa ya walinzi wa Simba kuweza kuifungia timu yao
Matokeo hayo yanaendelea kuiweka Simba kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya alama tisa baada ya kufikisha alama 44