Tangu kocha Sven Vandenbroeck akabidhiwe timu mwishoni mwa mwezi Novemba 2019, kasi ya upachikaji mabao mshambuliaji Meddie Kagere imepungua
Inaelezwa sababu ni kutokana na mabadiliko ya mfumo wa uchezaji ambapo Sven hupendelea zaidi kutumia 4-3-3 mfumo ambao unaweka mshambuliaji mmoja mbele na viungo watano
Ilikuwa tofauti kwa kocha aliyemtangulia, Patrick Aussems ambaye alipendelea zaidi 4-4-2 ambapo muda mwingi Simba ilicheza na washambuliaji wawili
Wakati Bocco alipoumia, Aussems aliwatumia Kagere na Miraji pamoja
Hata hivyo pamoja na kasi yake kupungua, bado Kagere amekuwa na mchango katika kuwatengenezea nafasi wenzake
Mnyarwanda huyo amesema wanapoingia uwanjani lengo kuu ni kushinda bila ya kujali nani anafunga
"Kazi yangu kama mshambuliaji ni kuifungia timu mabao ili tupate ushindi, lakini sio jukumu langu pekee, ni timu nzima. Hivyo nikifunga nafurahi lakini hata akifunga mwingine nafurahi kwani lengo letu ni moja, " amesema