Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba Senzo Mazingisa ametoa ufafanuzi kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa Simba ilipaswa kupata asilimia 20 ya mauzo ya mshambuliaji Mbwana Samatta ambaye amesajiliwa na klabu ya Aston Villa akitokea KRC Genk
Samatta aliitumikia Simba kabla ya kuuzwa TP Mazembe ambapo katika mkataba wake kulikuwa na kipengele ambacho kiliipa Simba haki ya kupata sehemu ya mauzo yake pale atakapouzwa kwa timu nyingine
Hata hivyo Mazingisa amefafanua kuwa mkataba huo ulikuwa kati ya Simba na TP Mazembe na ulimalizika baada ya Mazembe kumuuza Samatta KRC Genk
Mtendaji huyo wa Simba amesema mabingwa hao wa nchi walipata mgao wao wakati Samatta alipouzwa kwenda KRC Genk na mambo yaliishia hapo
"Hakuna kitu kama hicho (Simba kupata asilimia ya fedha ya uhamisho wa Samatta toka Genk kwenda Aston Villa). Mkataba huo wa 20% ulikuwa kati ya Simba na TP Mazembe, na uliisha Mazembe walipomuuza Samatta kwenda Genk."