Ukweli ni kwamba klabu ya Simba ndio timu iliyokamilika zaidi kwenye eneo la kiungo kuliko timu nyingine zinazoshiriki ligi kuu mismu huu
Ikiwa imewaongeza Luis Miquissone na Shiza Kichuya kwenye usajili wa dirisha dogo, Simba sasa imesheheni mafundi kwelikweli jambo ambalo litawapa mtihani wakufunzi wa timu hiyo Sven Vandenbroeck na Selemani Matola
Hata kabla ya kuwaongeza Kichuya na Miquissone, vita ya kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza haikuwa nyepesi
Wachezaji Francis Kahata, Hassan Dilunga, Miraji Athumani, Ibrahim Ajib na Clatous Chama wamekuwa wakichuana vikali katika eneo la kiungo mshambuliaji
Ujio wa Kichuya na Miquissone unakwenda kukoleza ushindani katika eneo hilo
Kichuya, Miquissone, Kahata kazi ipo
Nyota hawa huenda wakawa na ushindani wa kipekee kwani wana vitu vingi vinavyofanana
Wote wanatumia miguu ya kushoto, wabunifu na hodari wa kutengeneza nafasi huku Miquissone akiwa na takwimu nzuri zaidi katika kuzifumania nyavu


Kichuya anafahamika kwa uwezo wake mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao
Msimu wa 2017-18 alitengeneza mabao 26. Kahata msimu huu tayari amehusika kwenye mabao matatu ya Simba huku mwenyewe akifunga mawili
Kazi itabaki kwa benchi la ufundi kuwatumia ili wawe na manufaa kwa timu