Mabingwa wa nchi Simba leo saa 11 jioni watakuwa dimba la Taifa kuwakabili watani zao wa jadi Yanga katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Huo utakuwa mchezo wa kwanza kwa kocha Sven Vandenbroeck ambaye tangu atue Simba mwezi uliopita, ameweza kushinda mechi zote
Ni mchezo ambao Simba itaingia ikiwa na utulivu mkubwa kutokana na matokeo mazuri ambayo wameendelea kupata
Simba imeshinda michezo yote minne iliyopita, wakifunga mabao 14 bila ya kuruhusu bao hata moja
Wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi, ushindi kwao utazidi kuwaimarisha katika nafasi hiyo
Lakini kubwa zaidi, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Simba imekuwa bora zaidi dhidi ya Yanga
Kwani tangu mwaka 2015 Simba haijapoteza mchezo wowote pale ilipokutana na Yanga
Msimu uliopita mchezo wa kwanza ulimalizika kwa suluhu ya bila kufungana lakini mchezo wa pili Simba ikaibuka na ushndi wa bao 1-0
Wengi wanatarajia hakutakuwa na mabadiliko msimu huu kutokana na uimara wa kikosi cha Simba ukilinganisha na wapinzani wao
Ndio maana utaona mashabiki wa Simba hawana presha sana kuelekea mchezo huo ukilinganisha na wenzao wa Yanga
Kwani Yanga wanafahamu timu yao kama haitacheza kwa tahadhari leo, majanga yanaweza kuwakumba
Hata hivyo Msemaji wa Simba Haji Manara amesema pamoja na timu yake kupewa nafasi ya kushinda leo, lakini hawatawadharau wapinzani wao kwani wanafahamu michezo ya dabi wakati mwingine hutoa matokeo yasiyotarajiwa