Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amewatuliza mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaeleza watulie na katika hili dirisha dogo la usajili watamnasa winga wa UD Songo Luis Jose Miquissone na kilichobaki mbele yao kukamilisha tu mambo ya msingi
Senzo alisema ameona spidi za timu nyingine za Ligi Kuu Bara katika kufanya usajili ila wao waliamua kukaa kimya kutokana timu yao haina mahitaji makubwa ya wachezaji wapya wa kuwaongeza zaidi ya kuimarisha tu kikosi.
"Kuhusu hilo suala la usajili wa Miquissone, lipo kweli katika timu yetu na tulianza kulifanyia kazi kabla ya mimi kuwa katika nafasi hii ya utendaji na ambacho nataka kuwaeleza mashabiki watulie muda wowote tunakamilisha usajili wake," alisema.
"Nafahamu mashabiki wa Simba wanatamani kumuona Miquissone akiwa katika kikosi cha Simba ndio maana tunafata taratibu za msingi ili kuweza kumchukua na siku si nyingi tutawaeleza ambapo tumefika katika usajili wake.
"Kabla ya kuja hapa Simba Mtendaji aliyepita alikuwa ameshaanza kuongea na Miquissone na walikubaliana katika maeneo fulani ambayo tumeyawekea nguvu ili kulimaliza suala hili kwani tunafahamu ni mchezaji mzuri ambaye atakuja kuongeza nguvu katika kikosi chetu kwa maana hiyo mashabiki watulie," alisema Senzo