Baada ya timu yake kuingia hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoendelea nchini Uganda, Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars ya Tanzania Bara, Juma Mgunda, amesema wataingia na mbinu tofauti kuwakabili wenyeji Uganda katika mchezo huo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa KCCA.
Kilimanjaro Stars ilimaliza katika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne nyuma ya vinara wa Kundi B, Kenya ambao wamemaliza hatua ya makundi kwa kushinda mechi zote tatu, Zanzibar (Zanzibar Heroes) na Sudan, ndio zimeyaaga mashindano hayo kutoka kwenye kundi hilo.
Katika Kundi A, tayari wenyeji wenye pointi tisa, wameshaongoza kundi hilo hata kabla ya kumaliza mechi za mwisho jana jioni.
Mgunda amesema anatarajia mechi hiyo itakuwa ngumu na yenye ushindani kwa sababu timu zote zinaundwa na wachezaji wenye uzoefu na mashindano haya.
Mgunda alisema atawaandaa wachezaji wake kuingia uwanjani kwa tahadhari kwa sababu wanahitaji kupata matokeo mazuri na hatimaye kutinga fainali.
"Tunajua mechi ijayo itakuwa ngumu, yenye ushindani, lakini tutacheza kwa mipango na mikakati tofauti, tunahitaji kupata ushindi na si matokeo mengine, tutajipanga kupambana hadi mwisho," alisema Mgunda.
Aliongeza kuwa wachezaji wake wanaendelea kuimarika na kucheza katika kiwango cha juu ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao waliyojiwekea wakati wanakuja kwenye michuano hii.
"Tunamshukuru Mungu tumepata nafasi hii, katika kundi letu timu zote zilikuwa na nafasi ya kusonga mbele, sasa tunakwenda kucheza na wenyeji (Uganda), itakuwa mechi ngumu, yenye ushindani, lakini yote kwa yote tutaingia kupambana mpaka dakika ya mwisho," alisema Mgunda.
Aliongeza kuwa wanahitaji kuongeza umakini kwa kutumia vizuri nafasi zote watakazozitengeneza katika mechi hiyo ya hatua ya nusu fainali, tofauti na ilivyojitokeza kwenye mhezo wao dhidi ya Sudan ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.
Mara ya mwisho kwa Kilimanjaro Stars kutwaa ubingwa wa mashindano hayo ya Chalenji ilikuwa mwaka 2010, wakiwa nyumbani jijini Dar es Salaam baada ya kuwafunga Rwanda (Amabuvi), mabao 2-1.