Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems anaendea na program za kukinoa kikosi cha timu hiyo baada ya kurejea jana alfajiri
Mtendaji Mkuu wa Simba Senzo Mazingisa amesema kwa sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo wa ligi kuu kesho dhidi ya Ruvu Shooting na wanategemea Aussems ataiongoza timu
Aidha jana jioni Mazingisa pamoja na Kaimu Mwenyekiti wa Simba Mwina Kaduguda walipaswa kuwa na kikao na Aussems
Hata hivyo kikao hicho hakikufanyika
Akihojiwa na redio ya Wasafi mapema leo, Kaduguda alisema Aussems ndiye aliyekwamisha kikao hicho kwa kushindwa kuhudhuria licha ya kupewa taarifa mapema
Kaduguda alisema kocha huyo 'amelewa mafanikio' ndio maana alipuuza wito huo wa mabosi wake
CEO wa Simba Mazingisa alisema klabu haiwezi kuzungumza lolote wakati huu kutokana na kukabiliwa na mchezo dhidi ya Ruvu Shooting
"Kwa sasa hatutatoa kauli yoyote kuhusu masuala ya kocha (Aussems), tuna mchezo muhimu dhidi ya Ruvu Shooting, kocha wetu yuko na timu," alisema Mazingisa
Aussems ahusishwa na Polokwane City
Katika hatua nyingine, mtandao wa FarPost wa Afrika Kusini, umeripoti kuwa klabu ya Polokwane City inayoshiriki ligi kuu nchini humo imefanya mazugumzo na Aussems
Timu hiyo ilimtimua kocha wake mapema mwezi huu ambapo mtandao huo umebainisha kuwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo Johnny Mogaladi amemfanya Aussems kuwa chaguo lake la kwanza
Jana baada ya kusimamia mazoezi ya asubuhi, Aussems hakuwa tayari kuweka wazi juu ya safari yake
"Ni masuala binafasi. Inawezekana nilikwenda Uingereza kuzungumza na Tottenham kuhusu nafasi ya kuwa kocha wao lakini imekuwa bahati mbaya wamemchukua Mourinho," Aussems alitania
Hii itakuwa mara ya pili Polokwane City inatua Simba. Mwanzoni mwa msimu ilijaribu kumsajili nahodha wa mabingwa hao wa Tanzania Bara John Bocco lakini hawakufanikiwa baada ya kubainika kuwa walimsainisha Bocco mkataba wa awali