Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na presha inayoelekezwa kwa kocha Patrick Aussems licha ya kuwa bado hana msimu mbaya
Ukiondoa kilichotokea kwenye michuano ya ligi ya mabingwa mwanzoni mwa msimu, kwenye ligi Aussems ameiongoza Simba kushinda michezo saba kati ya tisa waliyocheza na kuiwezesha Simba kukaa kileleni
Matokeo ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mwadui Fc na suluhu ya bila kufungana dhidi ya Tanzania Prisons, ndio ambayo baadhi wanayatumia kumuhukumu
Lakini wanasahau Aussems aliiongoza Simba kutofungwa katika michezo 16 mfululizo!
Katika soka kuna wakati matokeo tofauti na ushindi lazima yatokee
Hakuna timu ambayo itashinda mechi zake zote kila siku. Kipindi kizuri kinaweza kuwa kirefu lakini lazima nyakati mbaya zitatokea
Ni wakati huo ambao umakini unahitaji kwani makosa madogo yanaweza kuigharimu zaidi timu
Ni bahati mbaya kwa hapa Tanzania mashabiki tumejiwekea utamaduni kuwa timu zetu lazima zishinde kila mchezo
Kocha anaweza kuiongoza timu kushinda mechi 10 mfululizo lakini akifungwa kwenye mchezo wa 11 mashabiki watamuona hafai
Presha huanzia kwa mashabiki, baadae itawakumba na viongozi ambapo wanajikuta wanafanya maamuzi ambayo hayana faida
Kwa sasa ni mapema sana kumuweka kwenye presha kocha Patrick Aussems kwani mpaka sasa ametimiza wajibu wake vizuri
Msimu uliopita ulikuwa msimu mzuri sana kwa Simba, kucheza robo fainali ligi ya mabingwa na kutwaa ubingwa wa ligi kuu yalikuwa mafanikio makubwa kwa Aussems na kikosi chake
Msimu huu haukuwa mzuri kwenye michuano ya Kimataifa lakini sababu za kutolewa mapema zipo, lakini kwenye ligi mpaka sasa ameiweka Simba kileleni mwa msimamo ikiwa imejikusanyia alama 22