Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa Juma Mgunda amesema suala la kuachwa mlinda lango Aishi Manula kwenye timu ya Taifa lisifanywe kuwa suala kubwa kwani ni jambo la kawaida
Manula amekuwa kipa namba moja wa timu ya Taifa kwa muda mrefu lakini tangu kumalizika kwa michuano ya Afcon 2019 iliyofanyika nchini Misri, Manula hajaitumikia Stars
Aidha mwanzoni mwa msimu alipata majeraha ambayo yalipelekea aondolewe kikosi cha Stars na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Kaseja
"Mchezaji yeyote ambaye ni Mtanzania ana haki ya kuitwa timu ya Taifa. Kukosekana kwa Manula ni jambo la kawaida kwani hata wakati yeye anaitwa wenzake hawakuwa wakiitwa," amesema
"Benchi la ufundi tumeridhishwa na uwezo wa makipa walioitwa hivyo tunapaswa tuwaunge mkono ili waweze kufanya vizuri"
Walinda lango walioitwa kwa ajili ya michezo miwili ya kusaka tiketi ya Afcon ni Juma Kaseja (KMC), Metacha Mnata(Yanga) na David Kissu anayechezea Gor Mahia ya Kenya
Kwa sasa Manula yuko 'fit' baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakimsumbua, ameendelea kujiimarisha na kurejesha ubora wake
Hakuna shaka bado nafasi yake ya kuitumikia Stars siku za usoni ipo