Pamoja na kuwakosa nyota wake 10, kikosi cha Simba kesho kinatarajiwa kurejea mazoezi kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting ambao utapigwa Novemba 24 uwanja wa Uhuru
Kocha wa viungo wa Simba Adel Zrane amesema wameandaa program maalum ili kuwaweka sawa wachezaji kipindi hiki ambacho ligi imesimama
Vinara hao wa ligi kuu wanarejea mazoezi baada ya mapumziko ya siku tatu waliyopewa na kocha Patrick Aussems siku ya Ijumaa
Huenda Simba ikacheza mechi kadhaa za kirafiki, ukiwa ni utaratibu uliopendekezwa na Aussems wakati ligi inaposimama kwa muda mrefu
Aidha kutokana na nyota wake wengi kuitwa timu za Taifa, baadhi ya wachezaji wa timu ya vijana (Simba B), watajumuishwa kwenye kikosi cha kwanza
Wachezaji walioitwa timu za Taifa ni Clatous Chama (Zambia), Sharaff Shiboub (Sudan) na Meddie Kagere (Rwanda)
Wengine ni Gadiel Michael, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Miraji Athumani na Hassan Dilunga walioitwa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'