Bado haijafahamika ni lini mshambuliaji John Bocco ambaye ni nahodha wa kikosi cha Simba atarejea kikosini
Bocco amekuwa nje ya uwanja kwa karibu miezi mitatu sasa akisumbuliwa na majeraha ya goti yaliyomuweka nje tangu August 17 akiumia katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam Fc
Kwa nyakati tofauti, Bocco alianza mazoezi mepesi lakini baadae kurejeshwa tena kitandani kuendelea na matibabu baada ya kubainika hakuwa amepona vizuri
Wiki iliyopita alifufua matumaini baada ya kuanza tena mazoezi mepesi
Hata hivyo kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema mshambuliaji huyo atahitaji muda zaidi kuweza kuwa sawa
Kwa michezo ya karibuni, ukiondoa mchezo dhidi ya Mbeya City, Simba inakabiliwa na changamoto ya kufunga mabao
Meddie Kagere ndiye anayetegemewa zaidi kufunga lakini kasi yake inaonekana kupungua mechi za hivi karibuni
Hii inatokana na kukamiliwa na walinzi wa timu pinzani baada ya kubaini ndiye mfungaji wa mabao karibu yote ya Simba akisaidiwa na Miraji Athumani
Kagere amefunga mabao nane wakati Miraji amepachika mabao manne
Msimu uliopita, Simba ikiwa na Bocco, Kagere na Okwi ilikuwa haikamatiki katika kuzifumania nyavu
Kuondoka kwa Okwi, kuumia kwa Bocco ni dhahiri kumechangia kupungua kwa idadi ya mabao Msimbazi
Uongozi wa Simba umepanga kutumia dirisha dogo la usajili kuongeza mshambuliaji mwingine. Uamuzi huu utakuwa na manufaa kwa mabingwa hao wa Tanzania Bara