Meneja wa klabu ya Simba Patrick Rweyemamu amesema kikosi cha timu hiyo kitaikabili Tanzania Prisons kwa tahadhari kubwa huku wakiwa na lengo la kuibuka na ushindi
Akizungumza mapame leo baada ya mazoezi ya mwisho ya Simba ambayo yalifanyika uwanja wa Uhuru, Rweyemamu amesema wanawaheshimu wapinzani wao lakini lengo lao kuu ni kuondoka na alama tatu
"Sisi ni kawaida yetu kuziheshimu timu zote tunazopambana nazo bila ya kujali matokeo ya mwisho ambayo wanakuwa wameyapata"
"Mwadui Fc hawakuwa vizuri sana wakati tunakutana nao lakini walitufunga licha ya kuwa tulitoka kushinda mechi tano mfululizo"
"Hatutawadharau, sisi lengo letu kuu ni kutwaa ubingwa. Na ili uwe bingwa lazima uwe na pointi nyingi, hivyo pointi tatu za mchezo wa kesho tunazihitaji ili kujiweka katika mazingira mazuri zaidi," amesema
Simba itachuana na Tanzania Prisons kesho katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Uhuru
Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza msimu huu zikiwa na rekodi tofauti
Simba wameshinda mechi saba kati ya nane walizocheza, wakifungwa mchezo mmoja wakati Prisons wameshinda mechi tatu kati ya tisa walizocheza, wametoka sare mara sita na hawajapoteza mchezo