Mabingwa watetezi Ligi Kuu ya Tanzania Bara Simba kesho Alhamisi watashuka uwanja wa Uhuru kuendelea na kampeni ya kusaka ubingwa wa tatu mfululizo kwa kuikaribisha Tanzania Prisons
Baada ya ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Mbeya City, Simba itakuwa na nafasi ya kujikita zaidi kileleni kama itashinda mchezo huo
Hata hivyo hautakuwa mchezo mwepesi hasa kutokana na uimara wa kikosi cha Tanzania Prisons msimu huu
Prisons inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 15 baada ya kushuka dimbani mara tisa
Ndio timu pekee ambayo bado haijafungwa mpaka sasa msimu huu, imeshinda mechi tatu na kutoka sare mechi sita
Hata hivyo itakutana na 'mziki' wa Simba ambao timu saba tayari zimeshindwa kuucheza
Aidha, mchezo huo kupigwa katika uwanja wa Uhuru ni faida nyingine kwa Simba ambayo imekuwa haifanyi makosa inapocheza nyumbani
Simba imeshinda mechi zote walizocheza uwanja wa nyumbani, hakuna shaka, wanaweza kuendeleza rekodi hiyo kesho
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema mchezo utakuwa tofauti kutokana na aina ya uchezaji wa Prisons
Lakini wamefanya maandalizi mazuri, wana uhakika wa kuondoka na alama zote tatu
Baada ya michezo hiyo ya mzunguuko wa 10, ligi itasimama kupisha michezo ya kalenda ya CAF ambayo ni ya kusaka nafasi ya kutinga fainali za Afcon 2021