Ripoti ya masuala yote ya mazoezi na program mbalimbali za kikosi cha Simba, itakuwa ikiwasilishwa moja kwa moja kwa Mtendaji Mkuu wa Simba Senzo Mazingisa
Mazingisa amekuwa makini kwenye usimamizi wa timu tangu alipokabidhiwa majukumu hayo kutoka kwa Crescentius Magori
Bosi huyo raia wa Afrika Kusini amemuagiza kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems kumpatia ripoti za kila kinachoendelea kwenye mazoezi ya Simba
Mazingisa ameahidi kumfuatilia mchezaji mmoja mmoja kulingana na ripoti hizo
Aidha, katika kuhakikisha kila mchezaji anawajibika ndani ya Simba, Aussems ametakiwa pia kuonyesha na kueleza sababu za baadhi ya wachezaji kutumika mara kwa mara huku wengine wakisugua benchi.
"Ripoti hiyo ya Aussems mbali ya mambo hayo, pia anatakiwa kuonyesha lini timu inaingia kambini kulingana na mchezo uliopo mbele yao, kwa nini wachezaji wanatumika zaidi ya wengine," Mmoja wa viongozi wa Simba amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
"Katika hili la wachezaji wasiotumika mara kwa mara kama Yusuph Mlipili na Ali Salim (hawajacheza mechi hata moja ya ligi) anatakiwa kueleza kwa sababu za kutowatumia ili kama wana mapungufu waambiwe wajirekebishe"
"Mazingisa anaamini timu ina kikosi kipana na wachezaji wana uwezo wa kushindana na kupata matokeo mazuri na ikitokea tumepoteza mchezo kama ilivyokuwa dhidi ya Mwadui, Aussems anatakiwa kueleza sababu"
Kumekuwa na malalamiko kuwa kwa Wanasimba wengi kwa nini kocha hamtumii mlinda lango Beno Kakolanya licha ya mlinda lango namba moja Aishi Manula kucheza chini ya kiwango kwenye baadhi ya mechi
Pengine kupitia utaratibu huu kocha atalazimika kumtumia katika baadhi ya michezo au kutoa sababu kwa nini hachezeshwi