Baada ya kupoteza mchezo uliopita kwa kufungwa bao 1-0 na Mwadui Fc, mabingwa watetezi ligi kuu, Simba leo wako dimba la nyumbani wakiikaribisha Mbeya City katika mchezo utakaopigwa saa kumi jioni kwenye uwanja wa Uhuru
Simba vinara wa ligi, watakuwa na nafasi ya kujichimbia zaidi kileleni kama watashinda mchezo huo
Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema kikosi chake kiko tayari, wana matumaini makubwa ya kushinda
Aidha Aussems amethibitisha kuwa walinzi Shomari Kapombe na Mohammed Hussein 'Tshabalala' ambao walikuwa majeruhi, wamepona na wanaweza kuwemo kwenye kikosi kinachoshuka dimbani leo
Tshabalala ambaye ni nahodha msaidizi wa Simba, amesema wameuchukulia mchezo huo kwa uzito mkubwa hasa baada ya kupoteza mchezo uliopita
Amesema kama wachezaji walikaa na kutathmini matokeo ya mchezo uliopita, wamekubaliana kutorudia makosa yaliyotokea mkoani Shinyanga
Mbeya City iko jijini Dar es salaam kwa siku tatu ikitokea mkoani Mwanza ambako iliifunga Mbao Fc na kulazimisha suluhu ya bila kufungana dhidi ya Alliance Fc
Timu hiyo imeshinda mchezo mmoja, imefungwa miwili na michezo mingine mitano imepata matokeo ya sare