Pamoja na kusema kuwa kikosi chake kimejiandaa kuwakabili mabingwa watetezi Simba kwenye mchezo wa ligi kuu kesho, kocha Mkuu wa Mbeya City Juma Mwambusi amesema timu yake ina wachezaji wengi wachanga
Simba na Mbeya City zitachuana kesho Jumapili kwenye mchezo wa ligi kuu ambao utapigwa uwanja wa Uhuru
Mchezo uliopita, Simba ilifungwa bao 1-0 na Mwadui Fc wakati Mbeya City ililazimishwa suluhu ya bila ya kufungana dhidi ya Allince Fc iliyomaliza na wachezaji tisa uwanjani baada ya wachezaji wake wawili kupewa kadi nyekundu
Ni mchezo ambao Simba itahitaji kushinda ili kulinda kampeni yake ya kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo
Mwambusi amesema anafahamu mchezo hautakuwa mwepesi lakini amewaandaa vijana wake kupambana

"Ligi ni ngumu sana, na mimi nina wachezaji wachanga, ndio ninakijenga kikosi, hata ile Mbeya City iliyokuwa tishio, nilitumia miaka miwili kuifikisha pale, haikutokea tu kibahati, iliandaliwa vema, naamini kikosi hiki pia kikiendelea kukaa pamoja, tutasumbua huko mbele," amesema
"Tunawaheshimu Simba, wana kikosi kizuri, lakini nimewaambia wachezaji wangu wacheze kwa nidhamu na bila ya woga"
Msimu uliopita Simba ilishinda michezo yote miwili dhidi ya Mbeya City, hakuna shaka msimu huu lengo la kocha Patrick Aussems ni kuendeleza rekodi hiyo