Kasi ya kikosi cha Simba imeanza kuzitia hofu timu zinazoshiriki ligi kuu ambapo kocha wa Mbao Fc Hemed Morocco amekiri kuwa na wakati mgumu kujiandaa kuwazuia mabingwa hao wa Tanzania Bara
Simba inarejea kanda ya ziwa kwa mara ya pili, ambapo keshokutwa Oktoba 30 itacheza na Mwadui Fc mkoani Shinyanga kisha kuifuata Mbao Fc huko Mwanza
Morocco amesema Simba ina kikosi kipana na bora tofauti na timu alizotangulia kucheza nazo, hivyo haitakuwa rahisi kuwakabili
"Katika msimu huu, Simba ndiyo timu yenye kikosi kizuri na kipana na kila anayekutana naye lazima afungwe, hivyo hata mimi napaswa kuifikiria, bila shaka akili yangu itatulia baada ya kucheza nayo na nisipojipanga tunaweza kuja kufungwa," alisema Morocco
Mchezo dhidi ya Mbao Fc una umuhimu wa kipekee kwa Simba hasa ikizingatiwa Mbao Fc ni moja ya timu zilizoifunga Simba msimu uliopita
Tayari Simba imeshalipa kisasi kwa Kagera Sugar kwa kuichapa mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa mwezi uliopita mkoani Kagera