Baada ya juzi kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam Fc, mabingwa wa nchi Simba wanaelekea mkoani Arusha ambako Jumapili wanakabiliwa na mchezo dhidi ya Singida United
Kulingana na ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi, Simba inakabiliwa na mechi mbili ndani ya siku tano
Kwani baada ya mchezo dhidi ya Singida United, Simba itaelekea mkoani Shinyanga kuifuata Mwadui tayari kwa mchezo utakaopigwa uwanja wa CCM Kambarage Oktoba 30
Aussems atamba, timu itafanya vizuri
Pamoja na ukaribu wa mechi hizo, kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems amesema wana matumaini watafanya vizuri
Mbelgiji huyo amesema kikosi chake kina wachezaji 27 ambao wote wanaweza kutimiza majukumu yao vyema
"Kila namba tuna wachezaji wawili au zaidi hivyo pamoja na kuwa ratiba sio rafiki sana, lakini tumejipanga kufanya vizuri. Tutaendelea na utaratibu wa kubadili kikosi mara kwa mara ili kuhakikisha wachezaji wote wanakuwa katika ubora unaotakiwa"
Simba ndio vinara wa ligi kuu wakiwa wamejikusanyia alama 15 wakishinda mechi zote walizocheza msimu huu