Kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Azam, Simba wameonyesha kuna kitu zaidi ya ushindi wanataka kukipata kutoka kwa Wanalambalamba hao.
Kwa mazoezi ambayo wamekuwa wakifanya tangu walipotolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba hawakuwa na haja ya kutumia nguvu nyingi kujipanga kwa ajili ya kusaka pointi tatu kwa timu za Ligi Kuu Bara.
Lakini kwa kinachoendelea Msimbazi, hasa wanapoisubiri Azam, ni wazi Simba mbali ya pointi tatu, wana mpango wa kuipa timu hiyo kipigo cha kihistoria na hatimaye kulisambaratisha benchi la ufundi la Wanalambalamba hao, nchini ya Kocha Mkuu wao, Etienne Ndayiragije.
Pamoja na kujifua hasa kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam, kikosi cha Simba kilicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Bandari ya Kenya, kabla ya kwenda mkoani Kigoma kunoa zaidi ‘makucha’ yao.
Tena safari hiyo ya Kigoma, ilimuhusisha Ofisa Mtendaji Mkuu wao, Senzo Mazingiza kuonyesha jinsi Wekundu wa Msimbazi hao wasivyotaka utani.
Kama hiyo haitoshi, pamoja na kujifua Gymkhana, kupiga tizi la nguvu Kigoma na kucheza mechi mbili za nguvu za kirafiki dhidi ya Mashujaa na Aigle Noir ya Burundi, mara baada ya kurejea Dar es Salaam jana, wachezaji wa timu hiyo wamepewa saa chache kabla ya kupelekwa mazoezini kujifua bila kujali kama kuna mvua zinazoendelea jijini.
Menaja wa Simba Patrick Rweyemamu, amesema hakuna kupumzika, kwa muda uliobaki wanatakiwa kuendelea na mazoezi leo kwenye Uwanja wa Uhuru, huku wakisubiri wachezaji wao waliopo timu za taifa.
"Tumemaliza salama ziara yetu ya Kigoma, tumecheza mechi mbili bila kupoteza, kitu ambacho tulikihitaji, tunawashukuru mashabiki wa Simba Kigoma kwa mapokezi na sapoti yao waliyoonyesha uwanjani.
"Tumerejea Dar es Salaam, mwalimu ataendelea na program yake ya maandalizi ya mechi yetu ya Ligi Kuu na Azam, kambini kama kawaida yetu, tutaingia siku mbili kabla ya mchezo,” alisema Rweyemamu.
Simba walikutana na Azam katika mchezo wa Ngao ya Jamii na kuibuka na ushindi wa mabao 4-2, mchezo uliopigwa Agosti 17, mwaka huu, kwenye Dimba la Uhuru, Dar es Salaam