Pamoja na kuwa nyuma kwa bao 1-0, kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kina matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo wa marudiano kusaka nafasi ya kucheza fainali za mashindano ya CHAN 2020 yanayohusisha wachezaji wa ndani
Kikosi cha Stars kiliwasili salama nchini Sudan jana kikitokea Rwanda ambako juzi walicheza mchezo wa kirafiki na kulazimishwa suluhu ya bila kufungana dhidi ya wenyeji wao Rwanda
Nahodha Msaidizi wa timu hiyo Erasto Nyoni amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri, jana jioni walifanya mazoezi yao ya kwanza nchini Sudan
Kuhusu usalama, Nyoni amesema timu iko katika mazingira salama huku akiwataka mashabiki kuwaombea ili waweze kushinda keshokutwa
Tanzania inahitaji kupata ushindi wa kuanzia mabao mawili ili kukata tiketi ya kucheza fainali za CHAN ambazo zitafanyika mwakani nchini Cameroon
Kama itafanikiwa kufuzu, hiyo itakuwa mara ya pili kwa Tanzania kushiriki fainali za michuano hiyo ikikata tiketi kwa mara ya kwanza mwaka 2006 wakati huo ikinolewa na Marcio Maximo raia wa Brazil
Awali mchezo huo ulitangazwa kuwa ungechezwa nchini Uganda kutokana na hofu ya usalama huko Sudan
Lakini wenyeji Sudan wamelihakikishia shirikisho la soka Barani Afrika (CAF) kuwa mchezo huo utachezwa nchini humo katika mazingira salama